JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania kuanzisha Kituo cha Ubunifu wa Kidijitali kwa Uratibu na Ushirikiano na ITU Geneva, Uswizi


Tanzania kuanzisha Kituo cha Ubunifu wa Kidijitali kwa Urati...

Na Mwandishi Wetu - GENEVA, Uswisi

Mkutano wa kwanza wa Bodi ya Ubunifu wa Kidijitali ya Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) umefanyika mjini Geneva tarehe 19-20 Machi, 2024. Katika Mkutano huo Tanzania imewakilishwa kikamilifu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Mwasaga na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta kutoka TCRA Mhandisi Mwesigwa Felician.

Miongoni mwa Manufaa muhimu ya ushiriki wa Tanzania kwenye bodi hiyo na hasa Mkutano huo ni pamoja na Tanzania kupata fursa ya kuanzisha kituo cha ubunifu kwa uratibu na ushirikiano kutoka ITU ambapo nchi itapata fursa ya kuendesha kituo kwa utalaamu wa kimkakati ili kuchochea mabadiliko ya ikolojia nzima ya bunifu za TEHAMA ndani ya nchi, kikanda na duniani kwa ujumla.

Akizungumzia Mkutano huo jana,  Mjumbe wa Bodi hiyo na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema kwambwa lengo la Mkutano huo ni kuzindua Bodi pamoja na kujadili kazi zitakazofanywa na Bodi pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya ubunifu wa kidigiti. 

“Hapa tumeangalia njia za kukuza bunifu mbalimbali za TEHAMA, kukuza ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya ubunifu na taasisi zinazojihusisha na ubunifu, tumeangalia namna tunavyoweza kuwa na mfumo utakaowezesha ubadilishanaji wa taarifa za vituo vya ubunifu Duniani,mambo ya haki-miliki za Ubunifu, ushirikishwaji wa Serikali katika kukuza ubunifu na vipaumbele katika ubunifu hasa bunifu zinazotatua changamoto za jamii,” alifafanua Dkt Bakari. 

Bodi ya Wadau wa Usimamizi wa Bunifu (ITU Innovation Board) inaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU Dkt. Cosmas Zavazava ambae ni Mwenyekiti ikiwa na wajumbe 23 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari ni miongoni mwa wajumbe wa bodi hiyo.  Pamoja na wajumbe wa nchi nyingine bara la Afrika linawakilishwa na wajumbe 8 kutoka nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria, Misri, Kenya, Zimbabwe, Gabon na Malawi.

Tanzania imepewa nafasi ya kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Ubunifu wa TEHAMA kitakachosimamiwa na Tume ya TEHAMA ikiwa ni sehemu ya Mtandao wa vituo vya ubunifu (ITU Acceleration Centres) ambavyo vimegawanywa kwenye ngazi ya Kidunia, Kikanda na Kitaifa ukiwa ni mkakati wa ITU kuhakikisha Ubunifu wa TEHAMA unahusika kuchagiza mapinduzi ya kiuchumi katika nchi wanachama ili kuchagiza ukuaji wa uchumi wa kidijiti. 

Bodi hiyo ya Ubunifu chini ya ITU ni miongoni mwa nyenzo tatu muhimu za wakfu wa Ushirikiano wa Ubunifu na Ujasirimali (Innovation and Enterprenuarship Alliance for Digital Development) ulioanzishwa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) Januari mwaka 2023, ukiwa na shabaha ya kuchagiza ubunifu wa kidijiti ambapo Shirika la Mawasiliano Duniani ITU limeweka bayana kupitia tovuti yake kwamba wajumbe wa Bodi hiyo ikiwemo Tanzania watakuwa ‘chachu muhimu’ ya kujenga mustakabali jumuishi wa kidijiti kwa watu wote, kwa kuwa wakfu wa ushirikiano huo unalenga kuharakisha mageuzi ya kidijiti kwa kuwezesha Ubunifu wa kidijiti na kuchagiza tunu za ujasiriamali kupitia bunifu hizo ambapo uwepo wa Tanzania unaipa fursa nchi kunufaika zaidi na maazimio ya kitaalamu kupitia jukwaa hilo.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!